Habari

RC Mara ataka Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kuibua fursa kwa ajili ya Maendeleo ya Mkoa

RC Mara ataka Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kuibua fursa kwa ajili ya Maendeleo ya Mkoa
Aug, 19 2024

Musoma, Mara

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ameitaka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Mkoa huo itakayoweka mikakati mizuri ya kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kuufanya Mkoa huo kupiga hatua ya kimaendeleo kwenye nyanja za kiuchumi na kijamii.

Mkuu wa Mkoa huyo ameyasema hayo tarehe 05/08/2024 wakati wa Kikao Kazi na Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi waliowasili Mkoani hapo kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kikanda, Mkoa na Wilaya.

Kanali Mtambi ameeleza kuwa kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji, Mkoa wa Mara unafursa za Utalii, Uchimbaji Madini, Ziwa Viktoria, Ufugaji na Kilimo ambazo bado hazijatumiwa ipasavyo ili kuweza kuleta maendeleo endelevu kwa jamii inayoishi kwenye Wilaya mbalimbali mkoani humo.

“Mkoa na Taifa kwa ujumla kuwa na Mpango wa Matumizi ya Ardhi ni muhimu, wakazi wengi wa Mkoa huu wanaishi maisha ya kawaida, ambayo hayawezi kumuendeleza mwananchi, fursa mbalimbali katika Mkoa wa Mara bado hazijatumika ipasavyo, zikitumika vizuri kupitia uwekezaji, utasaidia kuleta maendeleo” alisema Kanali Mtambi.

Aidha, Kanali Mtambi ameelezea matamanio ya Mkoa wake katika Mpango wa Matumizi ya Ardhi unaondaliwa ambayo ni pamoja na kuwa na eneo kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Kimataifa, maeneo ya ujenzi wa hoteli za nyota tano kwa ajili ya watalii wanaotembelea mbuga ya Serengeti pamoja na maeneo kwa ajili ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo pamoja na Mifugo.

Awali, Mratibu wa mradi wa ZORED unaowezesha kuandaliwa kwa mipango hiyo Bw. Nyerembe Munasa alieleza kuwa, wataalamu kutoka Tume wamewasili mkoani hapo kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika ngazi ya Kanda, Mkoa pamoja na Wilaya.

Kazi hiyo inawezeshwa na wataalamu kutoka Tume kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wale wa Halmashauri za Wilaya zilizopo katika Mkoa huo.

Kupitia Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Kikanda, Mkoa, Wilaya na Vijiji (ZORED), Tume inaandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Mkoa (Regional Land Use Framework Plan) ya Mikoa wa Mara, Shinyanga na Rukwa. Vilevile, jumla ya Halmashauri 4 katika Wilaya 2 za Bunda na Musoma, zinatarajiwa kuandaliwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kanda (Zonal Land Use Framework Plan) ili kuibua na kuziwekea mikakati ya matumizi fursa zilizopo katika ukanda wa Ziwa Viktoria

Aidha, zoezi linguine linalofanyika kupitia mradi huo ni uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya (District Land Use Framework Plan) ya Butiama pamoja na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 18 katika Halmashauri za Sumbawanga na Shinyanga.