Habari

Tume kuendesha oparesheni ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi Makete

Tume kuendesha oparesheni ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi Makete
Jun, 18 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Makete, imeanza kazi ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 44 wilayani humo ikiwa ni hatua ya awali kuelekea kupima maeneo na kuwamilikisha wananchi mashamba yao kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila.

Akizungumza kwenye Mkutano wa uzinduzi wa kazi hiyo uliowahusisha viongozi wa Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata pamoja na vijiji vyote vya Halmashauri ya Makete, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Antony Mtaka ameeleza matamanio yake ya kuona ardhi yote ya Makete imepangwa na kupimwa ili kufanya kilimo cha ngano kuwa na tija na kutoa mchango mkubwa wa uzalishaji wa zao hilo kwa Taifa.

“Kwa sasa tumeamua kutoa kipaumbele kwenye kilimo cha ngano na kwa kuwa Makete nzima imepimwa afya ya udongo, tunatakiwa kuzalisha sehemu ya ngano inayoagizwa kutoka nje ya nchi, na ili tufanikishe hilo ardhi yote ya Makete inatakiwa kupimwa na kila mwananchi awe na hatimiliki yake” alisema Mh. Mtaka

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari, ameipongeza Tume kwa kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 44 kwa wakati mmoja na kueleza kuwa ni hatua nzuri itakayosaidia kumaliza migogoro ya ardhi kwenye baadhi ya maeneo Wilayani humo.

“Tunaishukuru Tume kwa kuja kutupunguzia kazi, kuna baadhi ya maeneo yana migogoro ya ardhi ambayo imeshatufikia ofisini, ila kwa upangaji huu wa matumizi ya ardhi ya vijiji 44 kwa wakati mmoja, utatupunguzia migogoro ambayo tumekuwa tunahangaika nayo, na wananchi watajikita kwenye shughuli za maendeleo kutokana na ardhi yao kupimwa” alisema Bi. Judica Omari

Naye Mkurugenzi anayeshughulikia Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu kutoka Tume, Bw. Jonas Masingija Nestory amesema kuwa ufanyikaji wa kazi hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume kupitia fedha za miradi ya maendeleo.

Aidha, Mkurugenzi Masingija aliongeza kuwa mradi huo unalenga katika kuwezesha upangaji wa Matumizi ya Ardhi katika Vijiji na Wilaya zinazopitiwa na Miradi ya Kimkakati, Wilaya zilizopo mipakani pamoja na maeneo yenye migogoro ya matumizi ya ardhi.

“Katika utekelezaji wa mradi huu kwa upande wa Makete, jumla ya vijiji 44 vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi, ambapo kati ya hivyo, kuna vijiji vyenye vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji yake kwenye Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP), Vijiji vilivyotolewa maamuzi na Mawaziri wa Kista pamoja na Vijiji vyenye mashamba ya kilimo cha ngano” alisema Bw. Masingija

Vilevile, aliongeza kuwa, mara baada ya awamu ya kwanza ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji hivyo kukamilika, itafuata hatua ya pili ambapo kutaandaliwa Mipango Kina (Detail Land Use Plans) itakayowezesha wananchi kupimiwa mashamba yao na kupatiwa hati za hakimiliki za kimila.

Kwa hivi sasa kazi kama hiyo inatekelezwa katika Halmashauri nyingine 5 za Bunda, Iramba, Meatu, Itilima na Busega. Katika Halmashauri za Iramba na Bunda jumla ya vijiji 32 vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na kijiji kimoja kupimwa na kuandaliwahati za hakimiliki za kimila. Aidha, katika Halmashauri za Meatu, Itilima na Busega, jumla ya Hati za Hakimiliki za Kimila 7,500 zitatolewa kwa wananchi wa vijiji 25 ndani ya Wilaya hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Antony Mtaka (aliyesimama) akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Kupanga, Kupima Ardhi na kutoa Hatimiliki za Kimila kwa wananchi wa vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Makete

Mkurugenzi wa Usimamizi na Uratibu wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi (DLUPMC) kutoka Tume Bw. Jonas Masingija Nestory akiwasilisha Mpango Kazi wa namna Tume itakavyowezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji pamoja na upimaji wa mashamba na kutoa Hatimiliki za Kimila (CCROs)

Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa uzinduzi wa Upangaji, Upimaji Ardhi na Umilikishaji wakifuatilia kwa makini majadiliano wakati wa mkutano huo.

Wapima Ardhi kutoka Tume wakionesha vifaa vitakavyotumika kupima mashamba ya wananchi vijijini kwa ajili ya utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila

Wataalamu wa Tume pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Makete wakiwa kwenye kikao cha pamoja kujadili namna ya kutekeleza kazi ya upangaji na umilikishaji ardhi kwa wananchi