Habari
Tume Kuimarisha Ushirikiano na Wadau

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeanza kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali zikiwa ni jitihada za kuongeza kasi ya Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.
Jitihada hizo zimeanzishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph Mafuru kwa kufanya vikao na wadau waliopo Mkoani Arusha na kujadili fursa na maeneo ya ushirikiano na kuweka malengo ya pamoja ya ushirikiano wa kikazi baina ya Tume na Wadau hao.
Wadau waliotembelewa na kufanya vikao ni pamoja na Taasisi za African Wildlife Foundation (AWF), Tanzania Natural Resources Forum (TNRF), Frankfurt Zoological Society (FZS), Ujamaa Community Resource Team (UCRT, The Nature Conservancy (TNC) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Sura 116, katika utekelezaji wa majukumu yake, Tume inaweza kushirikiana na Taasisi/Mashirika yanayojihusisha na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na kuwa daraja la mawasiliano kati ya Serikali na Mashirika/Taasisi hizo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu ametembelea na kukagua Ofisi za Tume za Kanda ya Kaskazini zilizopo Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo na Watumishi wa Tume waliopo Kanda hiyo na kuweka mikakati itakayorahisisha utendaji kazi katika Mikoa inayohudumiwa na Kanda hiyo.