Habari

Tume na Ofisi ya Makamu wa Rais kuwezesha umilikishaji ardhi kulinda Mazingira

Tume na Ofisi ya Makamu wa Rais kuwezesha umilikishaji ardhi kulinda Mazingira
Oct, 25 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, imeanza kazi ya kuwezesha upimaji wa maeneo utakaopelekea utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi wa Vijiji vilivyopo katika Halmashauri 7 ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai Tanzania unaolenga katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira nchini.

Kazi hiyo ni muendelezo wa hatua ya 5 na 6 ya Upangaji Matumizi ya Ardhi inayohusisha Uandaaji wa Mipango Kina (Detail Land Use Planning) na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila ambapo hapo awali Vijiji vilivyopo ndani ya Halmashauri hizo viliandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyofanyika kuanzia hatua ya 1 hadi ya 4.

Kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini, kazi hiyo imeanzia Wilayani Mbeya, ambapo Wataalamu kutoka Tume wamewasili kwa ajili ya kuwezesha wananchi wa Vijiji 8 kupimiwa mashamba yao yanayopakana na maeneo ya Hifadhi ikiwemo misitu na vyanzo vya maji ili kuthibiti maeneo hayo yasiathiriwe na shughuli za kibinadamu

“Kimsingi, hatua hii inalenga kupunguza uvamizi wa maeneo ya Hifadhi hususani hifadhi za misitu na vyanzo vya maji, kwa sababu kama mtu atamilikishwa eneo lake, sio rahisi kuvamia au kwenda kuongeza eneo lake ndani ya misitu ya Hifadhi au vyanzo vya maji” alisema Pili Msati, Meneja wa Tume, Nyanda za juu Kusini

Uongozi wa Halmashauri ya Mbeya umesema kuwa, ujio wa Mradi huo utakuwa ni mkombozi kwenye dhana nzima ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira, kwa kuwa kila shughuli inayohusiana na ardhi itafanyika kwa mpangilio kutokana na shughuli iliyokusudiwa.

“Wananchi watakaopata hati hizi wahakikishe wanazitumia vizuri ili kujikomboa kiuchumi, lakini pia zitasaidia katika kulinda mazingira ikiwemo vyanzo vya maji na kwa kuwa hali ya mazingira kwa sasa duniani ni tishio, tukiyapima maeneo yetu na kuyatunza vizuri, yatatusaidia katika uhifadhi wa mazingira.” alisema Bw. Mohamed Aziz Fakiri, Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya

Kwa upande wao, wananchi wa Vijiji vinavyoguswa na zoezi hilo wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mpango huo wa umilikishaji maeneo kwani pamoja na kuimarisha uhifadhi, utasaidia pia kuepusha migogoro na mwingiliano wa matumizi ya ardhi.

“Nimefurahi hili zoezi, naona Serikali imetukumbuka kwa ajili ya kuepusha migogoro mbalimbali, pia na mimi nakuwa nimenufaika kwa sababu nakuwa nimemilikishwa ardhi kwa manufaa ya familia yangu, pili itatuepusha kuondokana na migogoro, na mazingira ambayo yapo jirani na Hifadhi” alieleza Philipo M. Menda, Mkazi wa Kijiji cha Mkuyuni

Kupitia Mradi wa Urejeshaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai Tanzania, zaidi ya Hati za Hakimiliki za Kimila 3,500 zitatolewa Vijijini katika Halmashauri za Mbarali, Iringa, Mbeya, Sumbawanga, Wanging’ombe, Tanganyika na Mpimbwe chini ya Ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Mazingira (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira.

Timu ya Wataalamu wa Tume wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya (wa 6 kutoka kulia) mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kuanza kazi ya kuwezesha wananchi wa Vijiji 8 katika Halmashauri hiyo kumiliki ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila

Wataalamu wa Tume wakiwa kwenye Kikao Kazi cha maandalizi ya utekelezaji wa kazi upimaji maeneo kwa ajili ya kumilikisha wananchi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila

Afisa TEHAMA Bw. Gerald Mseti (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo kwa wataalamu ya namna ya kupima na kuchukua taarifa za vipande vya ardhi kwa kutumia vishikwambi. Upimaji na Umilikishaji ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) unafanyika kupitia Mfumo wa Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUIS) uliosanifiwa na kutengenezwa na Tume.

Afisa Misitu Mwandamizi Bw. Emmanuel Malekanya (kulia) akitoa elimu ya uhifadhi katika Mkutano wa Kijiji cha Mkuyuni uliohusu uhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya kumilikisha ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila.

Sehemu wananchi wa Kijiji cha Mkuyuni wakijaza fomu za mombi kwa ajili ya kumilikishwa ardhi

Afisa Mipango Miji na Vijiji Bw. Jeremiah Marco akimpiga picha (passport size) mwananchi wa Kijiji cha Mkuyuni kwa ajili ya kuwekwa kwenye Hati mara baada ya kukamilisha kumpimia shamba lake.