Habari
Tume, TFS kulinda Misitu kupitia Mipango Shirikishi ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeingia makubaliano ya kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 vilivyopo kwenye ukanda wa misitu ya miombo hali itakayowezesha kulinda misitu hiyo na kufanya uhifadhi endelevu.
Akizungumza katika halfa fupi ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TFS Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Profesa Wakuru Magigi ameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya Taasisi za kisekta kwani kupitia mashirikano kama haya yanasaidia kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi.
“Kumekuwa na migogoro ya matumizi ya ardhi mingi sana katika maeneo mbalimbali ya hifadhi za misitu hapa nchini, sasa kupitia kazi hii tunaenda kuwawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo itawapelekea wananchi wenyewe kuwa walinzi namba moja wa misitu inayowazunguka kwenye Vijiji vyao” alisema Prof. Magigi.
Aidha kupitia kazi hii Profesa Magigi alihimiza kuwa wanaenda kuwezesha uandaaji wa mipango hiyo kupitia njia ya ushirikishwaji mkubwa wa wananchi wa vijiji hivyo hadi kwenye hatua ya umilikishwaji, na pindi watakapomilikishwa ardhi zao waweze kutumia ardhi hizo kujikwamua kiuchumi kutokana na shughuli mbalimbali zitakazoibuliwa kupitia Miradi ya Uhifadhi Misitu.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS Profesa Dos Santos Silayo ameeleza kuwa uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiji vinavyozunguka misitu ya hifadhi umekuwa na mafanikio makubwa, kwani imefanya maeneo mengi misitu kuwa salama kutokana na elimu ya uhifadhi waliopatiwa wananchi wakati wa mazoezi kama hayo.
“Tunaenda kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiji vinavyopitiwa na misitu ya miombo, kama mnavyojua, shughuli nyingi za kibinadamu zinafanyika katika maeneo pembezoni mwa misitu, sasa shughuli hizo zisiporatibiwa vizuri, misitu yote hapa nchini itateketea”, alisisitiza Prof Silayo.
Vilevile, Profesa Silayo aliongeza kuwa TFS itaendelea kushirikiana na Tume kupitia Miradi ya Kimkakati kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji vyote vyenye changamoto za muingiliano wa matumizi na misitu ya hifadhi. Aidha, alisisitiza kuwa kazi hii itaenda sambamba na utoaji elimu ya uhifadhi kwa wananchi ambayo itasaidia rasilimali ardhi kuwa salama na kila mmoja atafanya shughuli zake kwa utaratibu ili kusaidia kulinda misitu.
Kazi hii itafanyika, kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame Tanzania (Integrated Landscape Management in Dry Miombo Woodlands of Tanzania) kwenye Vijiji 14 vilivyopo katika Wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge Mkoani Tabora.