Habari

TUME, TFS Wapiga Kambi Tabora na Katavi Kuimarisha Uhifadhi wa Misitu ya Miombo

TUME, TFS Wapiga Kambi Tabora na Katavi Kuimarisha Uhifadhi wa Misitu ya Miombo
Oct, 14 2024

Na Claudius Masayanyika, Mlele, Katavi

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameanza kuwezesha uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 14 vinavyopakana na safu za misitu iliyopo kwenye ukanda wa Kaliua na Mlele (Kaliua and Mlele landscapes) katika Mikoa ya Tabora na Katavi ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame Tanzania (Integrated Landscape Management in Dry Miombo Woodlands of Tanzania).

Kazi hiyo inayofanyika kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya (Sikonge, Urambo, Kaliua na Mlele) inalenga katika kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa mazingira, ambayo ni muhimu kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu pamoja na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa ardhi na upotevu wa bioanuai.

Aidha, upangaji matumizi ya ardhi ya Vijiji hivyo utahusisha utoaji elimu kwa wananchi juu ya Sheria na Miongozo ya upangaji na usimamizi wa ardhi, usimamizi wa Maliasili na mazingira pamoja na kujengea uwezo timu za upangaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi za Wilaya, Vijiji pamoja na Mabaraza ya ardhi ya Vijiji kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi Vijijini.

Sambamba na hilo, kazi hizo zitaambatana na wananchi kwenye Vijiji husika kutunga Sheria ndogo za usimamizi wa maeneo yaliyotengwa, uhakiki wa mipaka kati ya Vijiji na Vijiji, Vijiji na hifadhi pamoja na kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi itakayobainika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wataalamu kutoka Tume na TFS wamesema kuwa kupitia uandaaji wa mipango ya matumizi itasaidia wananchi katika Vijiji hivyo kuondoa muingiliano ya kimatumizi kati ya shughuli za kibinadamu na hifadhi za misitu.

“Tunapoandaa mipango ya matumizi ya ardhi tunabainisha matumizi mbalimbali ikiwemo makazi, kilimo, malisho na mengineyo ikiwemo maeneo ya misitu, na hii misitu inasaidia kwa ajili ya shughuli nyingine kama vile ufugaji nyuki, na wananchi wengi wa huku wanafanya hii shughuli kwa hiyo kupitia mradi huu, utawasaidia wananchi kuhifadhi misitu kupitia shughuli mbadala za ufugaji nyuki katika misitu hiyo.” alisema Bw. Amos Mpuga, Mkuu wa Kanda (Kaskazini) kutoka Tume.

Aidha, Afisa Misitu Mkuu kutoka TFS Bi. Maria S. Kapina amesema kuwa, mradi unatilia mkazo katika kuhakikisha misitu aina ya miombo inaokolewa na anaamini kuwa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi itasaidia katika kurejesha misitu hiyo katika hali yake iliyokuwepo hapo awali kwa kuwa wananchi watafanya shughuli zao pasipo kuingilia hifadhi za misitu.

“Tume na TFS tupo kwenye Vijiji hivi 14 vya Wilaya 4 tunawezesha kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji hivi vilivyopakana na hifadhi ya misitu yenye uoto aina ya miombo, tukiwaongoza wananchi namna ya kutumia ardhi yao ili watenge maeneo ya kilimo, Malisho, pamoja na maeneo kwa ajili ya uhifadhi wa misitu ili wananchi hawa waje wanufaike na mazao ya misitu” alisema Mhifadhi Kapina na kusisitiza “tunatarajia mipango hii isaidie katika kuondoa muingiliano wa matumizi ndani ya misitu kwa kuwa wananchi watakuwa wanajua maeneo yao ya kilimo na malisho tofauti na hifadhi ambapo itapunguza uvamizi wa misitu.”

Naye Afisa Mipango Miji na Vijiji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Bw. Hussein Msumi ameishukuru TFS kwa kuleta mradi huo ambapo hapo awali, Halmashauri hiyo iliwezeshwa kupima mipaka ya Vijiji vinavyopakana na Misitu ya Hifadhi na sasa wanawezeshwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ili kupunguza shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya Hifadhi.

“Zoezi la kwanza tulipima mipaka ya Vijiji hivi, na kwa sasa tupo kwenye hatua ya kuviandalia mipango ya matumizi ya ardhi, na hii mipango itakuwa na faida kwa wananchi na uhifadhi kwani itapunguza msukumo wa kuingia kwenye hifadhi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji kwa kuwa matumizi hayo yatakuwa yametengwa kwenye ardhi ya Kijiji” alisema Bw. Msumi.

Kwa upande wao, wananchi wa Vijiji vinavyonufaika na zoezi hilo wameeleza utayari wao wa kushiriki katika zoezi hilo kwani wanaona kuna fursa nyingi zitapatikana mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo. Aidha, wananchi hao wamesema kukamilika kwa zoezi hilo pia kutawasaidia kuondokana na migogoro baina ya makundi mbalimbali pamoja na kuacha kufanya shughuli za kilimo na malisho ndani ya hifadhi.

“Kwa mpango huu wa matumizi bora ya ardhi utatusaidia kuepusha migogoro kati ya mwingiliano wa Kijiji na Kijiji, mkulima na mfugaji, hifadhi ya Taifa na kilimo, kwa hiyo mpango huu utatuweka pazuri kila mmoja ataelewa anapoanzia na anapoishia pasipo muingiliano” alisema Bw. Alfred Msuka, Mwenyekiti wa Kijiji cha Wachawaseme

Pindi zoezi hili litakapokamilika, wananchi wa Vijiji hivi watanufaika kwa kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi, kuwekeza miradi ya kudumu katika maeneo sahihi yaliyobainishwa na wananchi wenyewe, kuwa na Hati za kumiliki ardhi kwa mwananchi mmoja mmoja pamoja na kuanza kuwekeza miradi kama vile ya mnyororo wa ufugaji nyuki katika misitu iliyohifadhiwa na kuheshimiwa na wananchi wenyewe.

Mradi huo wa Miombo unatekelezwa katika ukanda wa Tabora (Kaliua landscape) na Katavi (Mlele Landscape) upo chini ya Wizara ya Maliasili kupitia TFS huku ikishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira kupitia Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) pamoja na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO).