Habari
TUME, USAID bega kwa bega katika Uhifadhi Maliasili
Juhudi za Tume kuimarisha ushirikiano na wadau zimeendelea kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Bw. Joseph C. Mafuru kukutana na kufanya mazungumzo na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na kukubaliana katika utekelezaji wa Miradi wa USAID – TUHIFADHI MALIASILI utakaosaidia katika kuimarisha Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.
Mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Kimataifa la Utafiti (Research Triangular Institute - RTI) unalenga katika kutoa masuluhisho yanayotegemea sayansi na huduma za kiufundi ili kuboresha maisha (Delivering science-based solutions and technical services to improve lives).
Aidha, Mradi umejikita zaidi katika kusaidia uhifadhi wa Maliasili, bioanuai , Urejeshaji ardhi iliyoharibika, Urejeshaji wa uoto wa asili, uhifadhi wa viumbe adimu ambapo kwa sasa unatekelezwa katika urejeshaji wa korido 7 zawanyama pori kama vile za Kwakuchinja ( Babati na Monduli), Korido ya Amani Nilo (Muheza), Burigi - Chato na nyinginezo.
Mipango ya Matumizi ya Ardhi ni sehemu ya majukumu yanayotekelezwa na Mradi huo ili kutimiza na kuimarisha malengo ya Uhifadhi nchini. Katika kuunga mkono juhudi za Uhifadhi wa Maliasili na Diplomasia ya Uchumi, Tume na USAID wamekubaliana kutekeleza sehemu ya Mradi huo kwa kuendelea kuwezesha utendaji kazi kupitia Mfumo wa Taarifa za Matumizi ya Ardhi (National Land Use Information System - NLUIS)
Sambamba na hilo, USAID TUHIFADHI MALIASILI imeahidi kuwezesha utoaji wa Elimu kwa Umma juu ya Mfumo huo, Kuwezesha Vifaa vya kisasa vya Tehama vitakavyosaidia kuongeza kasi ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi nchini pamoja na kushiriki kuwezesha vikao kazi na wadau waMipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.