Habari

Tume yaandika Historia Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji Wilayani Rombo

Tume yaandika Historia Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji Wilayani Rombo
Oct, 08 2024

Na Moteswa Msita, Rombo, Kilimanjaro

Kwa mara ya kwanza toka kuanzishwa kwake, Halmashauri ya Wilaya ya Rombo inapata neema ya kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kunakuwa na milki salama za ardhi, kuongeza uzalishaji wenye tija, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuzuia migogoro ya ardhi.

Hayo yamebainika Wilayani Rombo, Mkoani Kilimanjaro mara baada ya Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kuwasili Wilayani humo kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi nchini.

Akizungumza na Wataalamu hao, Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Kiseo Nzowa ameunga mkono jitihada za Serikali kupitia Tume na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikisha zoezi hilo la uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi katika Vijiji vilivyobainishwa.

Aidha kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe. Raymond Mwangwala amefurahishwa na ujio wa zoezi hilo huku akitambua kuwa uandaaji wa mipango ya matumizi husaidia kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi na kuchochea maendeleo endelevu katika Vijiji na Wilaya husika.

Katika hatua nyingine wataalamu kutoka Tume wameendesha mafunzo kwa Timu Shirikishi ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya (Participatory Land Use Management Team – PLUM) inayoundwa na wataalamu kutoka sekta mbalimbali zinazohusika na matumizi ya ardhi katika Halmashauri hiyo.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa mujibu wa Mwongozo wa Uandaaji na Usimamizi Shirikishi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji nchini (Guidelines for Participatory Village Land Use Planning, Administration and Management in Tanzania) ili kuwajengea uwezo timu ya PLUM kabla ya kuanza zoezi la Uandaaji wa Mpango wa matumizi ya Ardhi.