Habari
Tume Yafanikisha Upimaji wa Mipaka ya Vijiji Meatu
Vijiji vya Iramba Ndogo, Sungu, Mwanjoro na Jinamo vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu vimekamilisha upimaji wa mipaka ya vijiji vyao na kuahidi kuiheshimu mipaka hiyo ili kuepuka migogoro kwa kuwa ni makubaliano baina ya pande zote zinazohusika.
Upimaji wa mipaka hiyo umefanywa na Wapima Ardhi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) ambao pamoja na Wataalamu wengine wamepiga kambi Wilayani humo kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 12 katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
Akizungumza wakati wa zoezi la upimaji mpaka kati ya kijiji cha Mwanjoro na Jinamo, Mpima Ardhi kutoka Tume, Mikidadi Kalimang’asi amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi, upimaji wa mipaka ya vijiji ni lazma uwe shirikishi kwa kuwahusisha Halmashauri za Vijiji kwani wao ndio wasimamizi wa ardhi za vijiji.
Aidha, alieleza kuwa mara baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya mpaka baina pande zote za vijiji vinavyopakana, ni lazma kuwekwe alama za kudumu (beacon) na kuandika muhtasari kwa ajili ya kumbukumbu na kusajili mipaka hiyo.
“Tumekutana hapa kwa ajili ya kujadiliana juu ya mpaka wenu, kila upande inabidi useme kijiji chao kinaishia wapi, mkishakubaliana itabidi twende tukaweke alama za kudumu, alama za kudumu pia zinaweza kuwa maumbile ya asili ya kudumu kama vile mito au milima, sasa inategemea vijiji vyenu vinagawanyikia wapi” alieleza Bw. Mikidadi.
Kwa upande mwingine, mzozo uliibuka kati ya Vijiji vya Iramba Ndogo na Sungu ambapo kila kijiji kilivutia upande wake katika sehemu ambayo vijiji hivyo vinakutana na kugusa kwenye eneo la Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori (WMA). Aidha, kutokana na mzozo huo ilihitajika elimu ya ziada kutoka kwa Mpima wa Tume Bw. Emmanuel Kasitila ili kuweza kutafuta muafaka
“Hapa tunapoanzia panaleta shida, mmechukua muda mrefu kubishana lakini hakuna sababu ya kulumbana kwa kuwa endapo mtakubaliana wote mnafika kwenye hii Hifadhi, haijalishi unafika kwa ukubwa wa kiasi gani, kila kijiji kitatambulika kuwa kinafika Hifadhini, na kama kuna kunufaika wote mtanufaika sawa” alisema Bw. Kasitila
Mara baada ya kupatiwa elimu na wataalamu, wawakilishi vijiji hivyo walifikia muafaka na kusimika alama (beacon) kuashiria kuisha kwa kiu yao ya muda mrefu ya kutaka kupima mpaka huo.
Hapo awali, Vijiji vya Iramba Ndogo na Mwanjoro vilikuwa vijiji mama, ambapo katika miaka ya hivi karibu viligawanyika na kuanzishwa vijiji vya Sungu, kutoka Iramba Ndogo na Kijiji cha Jinamo kilichotoka katika Kijiji cha Mwanjoro.
Mpima kutoka Tume (aliyechuchumaa) Bw. Kasitila Emmanuel akiwaongoza wajumbe wa Kamati ya Mipaka kuchukukua jira (coordinates) za jiwe la mpaka linalotenganisha Vijiji vya Iramba Ndogo na Sungu
Mwenyekiti wa Kijiji cha Jinamo (Katikati) akisaini fomu na muhtasari wa makubaliano ya mpaka. Pembeni yake ni Maafisa Watendaji wa Vijiji vya Mwanjoro na Jinamo
Wajumbe kutoka vijiji vya Iramba Ndogo na Sungu na Mpima wa Tume wakifurahi mara baada ya kumaliza zoezi la kupima mpaka unaotenganisha vijiji hivyo