Habari

Tume Yakamilisha Rasimu ya Mwongozo wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji

Tume Yakamilisha Rasimu ya Mwongozo wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji
Nov, 19 2020

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Shirika la Care International Tanzania imekamilisha urejeaji wa Mwongozo Shirikishi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji (Guidelines for Participatory Village Land Use Planning, Management and Administration in Tanzania) unaotegemewa kuanza kutumika mapema kuanzia mwakani (2021).

Mwongozo huo ambao unaweka utaratibu wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, hutumika na wawezeshaji katika ngazi mbalimbali ili kuwawezesha wananchi wanaoishi vijijini kutumia rasilimali za ardhi katika mpangilio na ubora unaofaa kwa kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya ardhi kama vile kilimo, malisho, huduma za jamii na uhifadhi wa vyanzo maji, wanyamapori na misitu.

Akizungumza wakati wa kukamilisha kazi hiyo iliyofanywa na wataalamu na Tume kwa ushirikiana na wadau wengine, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Dkt. Stephen Nindi amesema urejeaji wa mwongozo umezingatia na kutoa mwongozo wa namna ya kupanga na kusimamia rasilimali za ardhi kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya jamii, mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira.

Naye mratibu wa programu ya Ardhi Yetu kutoka Shirika la Care International Tanzania, Bwana Alfei Maseke ameipongeza Tume na kuahidi kuendeleza ushirikiano kwani lengo la Shirika lao kwenye kazi hii ni kuona Mwongozo unakamilika katika hatua zinazofuata na kuanza kutumika ili vijiji vyote nchini viandaliwe mipango ya matumizi ya ardhi.

Mwongozo huu umerejewa ili kutambua na kuainisha masuala yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi, athari zake na namna ya kukabiliana nayo. Aidha, urejeaji wa Mwongozo huu ulilenga kuangalia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika usimamizi wa rasilimali za vijiji hasa kwa makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na kuangalia upya gharama na matumizi ya teknolojia katika upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.

Hatua inayofuata kabla ya kuanza kutumika kwa Mwongozo huo ni kuwakutanisha wadau wote (Wizara na Taasisi za Serikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali pamoja na Mashirika Binafsi) kwa ajili ya mapitio, uchambuzi na uthibitisho kabla ya kupelekwa kwenye Bodi ya Tume na baadae Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuridhia uanze kutumika.

Rasimu ya mwongozo huo inapatikana kwenye tovuti ya Tume kupitia kiunganishi https://www.nlupc.go.tz/publications/guidelines (Draft Guidelines for Participatory Village Land Use Planning, Management and Administration in Tanzania - 3rd Edition).