Habari
Tume yashiriki Mkutano kuhusu Shoroba za Wanyamapori
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeshiriki katika Mkutano wa Pili wa Mwaka kuhusu Shoroba za Wanyamapori (The 2nd National Annual Wildlife Corridors Forum 2024) uliohusisha Wadau mbalimbali kutoka Wizara za Kisekta na Taasisi zinazohusika na Maliasili pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Katika Mkutano huo uliofanyika Jijini Arusha, ulifunguliwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dustan Kitandula, Tume iliwasilisha mada iliyoangazia mchango wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika kulinda na kufufua Shoroba za Mapitio ya Wanyamapori.
Akiwasilisha mada hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti, Uzingatiaji na Mifumo ya Taarifa za Matumizi ya Ardhi kutoka Tume, Dkt. Joseph Paul amewafahamisha Wadau wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuwa mapema mwaka huu mwezi Aprili 2024, Wadau walipitia na kupitisha Miongozo ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ikiwemo Mwongozo wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi ya Pamoja kwa Vijiji vinavyozungukwa na rasilimali ya aina moja (Joint Village Land Use Planning Guidelines).
Pamoja na masuala mengine, Mwongozo huo umefafanua wazi juu ya kuyatambua maeneo mbalimbali ya Vijiji yenye rasilimali zinazotumiwa na zaidi ya eneo moja la kiutawala kama vile Nyanda za Malisho, vyanzo vya maji, Hifadhi pamoja na Shoroba za Wanyamapori ambazo huwezesha wanyama hao kupita kutoka kwenye hifadhi moja hadi nyingine.
Vilevile, katika kuhakikisha kunakuwa na Usimamizi na Utekelezaji wa matumizi ya ardhi yaliyotengwa, kila sekta zilizopo kwenye Mamlaka za upangaji, Miongozo inaelekeza kuandaa Mipango Kina (Detail Management Plans) ili kuyaendeleza maeneo hayo ikiwemo Shoroba za Wanyamapori kwa kuziandalia mipango na bajeti ya utekelezaji ikiwemo kuziwekeamiundombinu muhimu na kuyaepusha kuvamiwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.
Aidha wadau walihimizwa juu ya umuhimu wa kuzingatia Sheria na Miongozo iliyopo ya uandaaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi kama nyenzo muhimu ya Utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Mkutano huo wa siku tatu umemalizika kwa wadau hao kukaribishwa kushirikiana na Tume ikiwemo kufahamishwa fursa za ushirikiano kama vile masuala ya teknolojia, tafiti, kuwezesha mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi zote ikiwemo kuwezesha urejeaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Taifa ambao utaingiza masuala yote mtambuka ikiwemo mpango kutambua maeneo ya Uwekezaji, Miundombinu, Miradi ya Kimkakati na Shoroba za Wanyamapori.