Habari

Wahadhiri Chuo cha Twente Wakoshwa na Usimamizi wa Nyanda za Malisho Selela

Wahadhiri Chuo cha Twente Wakoshwa na Usimamizi wa Nyanda za Malisho Selela
Apr, 21 2026

Wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Twente nchini Uholanzi wameonesha kuridhishwa na namna jamii inavyosimamia nyanda za malisho katika Kijiji cha Selela, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, kufuatia ziara ya mafunzo iliyolenga kujionea utekelezaji wa mpango wa matumizi ya ardhi uliowezeshwa na Ujamaa Community Resource Team.

Katika ziara hiyo, wahadhiri hao, Dkt. Johannes Flacke na Andre da Silva Mano, walivutiwa na kiwango kikubwa cha ushirikishwaji wa jamii katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, hususan katika uandaaji wa ramani zinazoonesha mgawanyo wa matumizi mbalimbali ya ardhi. Walisema ushiriki huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uendelevu wa nyanda za malisho kupitia usimamizi shirikishi wa rasilimali hizo.

Aidha, walieleza kuwa uzoefu walioupata umeonesha umuhimu wa kuunganisha maarifa ya kijamii (social mapping) na teknolojia za kisasa ili kuboresha mchakato wa uchoraji wa ramani na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi na jumuishi kuhusu matumizi ya ardhi.

Wahadhiri hao walibainisha kuwa bado kuna fursa ya kuimarisha zaidi mifumo ya ukusanyaji na uchakataji wa takwimu, ikiwemo kubaini aina ya taarifa zinazopaswa kuchapishwa na namna zinavyoweza kutumiwa na wadau mbalimbali kwa manufaa ya maendeleo ya jamii.

Pia walisisitiza umuhimu wa kuendeleza matumizi ya ramani za kidijitali zitakazowezesha sekta mbalimbali kupata taarifa sahihi kuhusu rasilimali zilizopo katika ngazi ya kijiji, hatua itakayochochea upangaji bora na usimamizi endelevu wa ardhi.

Kwa upande mwingine, wahadhiri hao walionyesha utayari wao wa kushirikiana na taasisi za ndani katika kufanya tafiti, kutoa mafunzo na kubadilishana uzoefu ili kuboresha zaidi mifumo ya upangaji wa matumizi ya ardhi. Walisema ushirikiano huo utawezesha pia kuhamasisha utaalamu wa pamoja katika kutatua changamoto zilizopo.

Walihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuharakisha mchakato wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na kuhakikisha ramani za matumizi ya ardhi zinapatikana kwa maeneo yote nchini kwa ufanisi zaidi.

Ziara hiyo imeonesha wazi namna ushirikiano kati ya taasisi za kimataifa na jamii za ndani unavyoweza kuchangia katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kukuza maendeleoendelevu.