Habari
Upangaji wa Matumizi ya Ardhi, Upimaji wa Maeneo Msomera Waanza Tena

Awamu ya pili ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali pamoja na Upimaji wa maeneo kwa ajili ya Makazi na Mashamba ya wenyeji na wageni watakaohamia kutoka Hifadhi ya Ngorongoro umeanza katika Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kilichohusisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na wataalamu wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Albert Msando amewataka wataalamu hao kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kutatua changamoto zote za wakazi wa Msomera zinazatokana na matumizi ya Ardhi.
“Tumekuwa na imani na Tume kwa sababu kazi ya kwanza mliyoifanya imejitangaza na kujitosheleza, hivyo basi ikiwa Serikali imewaamini kuifanya kazi hii tena, ninapenda kuwaasa kuifanya kwa uangalifu na kwa maslahi mapana ya wananchi na tunaamini mnakwenda kutatua changamoto zote za ardhi zilizopo kwa wananchi waishio Msomera” alisema Mh. Msando.
Aidha, kuhusu changamoto ya umilikishaji ardhi na kupatiwa Hatimiliki za Kimila kwa wenyeji waishio Msomera Mh. Msando amesema ni lengo la Serikali kuwapatia Hatimiliki za Kimila wananchi wote waishio katika eneo la Msomera ili kuwahakikishia umiliki wa ardhi yao na ziwasaidie kuwainua kiuchumi.
“Tunatarajia mtatoa Hatimiliki za Kimila kwa wageni wanaohamia kutoka Hifadhi ya Ngorongoro, lakini pia tuhakikishe hawa waliokutwa na wageni wanapewa maeneo ya Makazi na Kilimo na kupatiwa Hatimiliki, tuna imani hili mtalifanya ndani ya muda ili kuanza kazi nyingine kubwa iliyopo mbele yenu” alisisitiza Mh. Msando.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Prof. Wakuru Magigi amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Handeni kuwa Kijiji cha Msomera kinakwenda kuwa kijiji cha mfano Tanzania kwa kupangwa maeneo ya matumizi ya aina zote ili kuendana na maisha ya kisasa na kuleta unafuu kwa wananchi.
“Kwa Upangaji huu wa Mji wa Msomera uliofanywa na wataalamu wetu tunatarajia Kijiji cha Msomera kuwa Kijiji cha mfano Tanzania na huenda Afrika kwani Upangaji wake umezingatia utaalamu wa hali ya juu na kukidhi mahitaji yote yanayohitajika kwa maisha ya sasa” alisema Prof. Magigi na kuongeza “Miundombinu imeboreshwa na huduma za jamii kufikika kwa urahisi, tunatarajia kuwa na shughuli za kilimo na ufugaji za kisasa ili kuleta tija kwa wananchi wa Msomera”.
Hapo awali, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ilipanga matumizi ya ardhi kwa ajili ya makazi, kilimo, huduma za jamii, nyanda za malisho, ushoroba wa wanyamapori pamoja na hifadhi ya vyanzo vya maji na misitu.
Aidha, katika upangaji huo wa awali, takribani nyumba 103 zilijengwa, kituo cha afya, shule ya Msingi na Sekondari pamoja na kuweka miundombinu kwenye maeneo ya malisho ikiwa ni muendelezo wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili kwa ajili ya makazi, huduma za jamii pamoja na nyanda za malisho.
Katika awamu ya pili, zoezi hili litahusisha kuwatambua wenyeji wa kijiji hicho, kuwapimia na kuwamilikisha maeneo yao, pamoja na kuanza upangaji na upimaji wa maeneo mapya ambayo yatamilikishwa kwa wageni wataohama kwa hiari yao kutoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Albert Msando akisisitiza jambo wakati akiongea na Viongozi na Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (hawapo pichani)
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Prof. Wakuru Magigi (wa pili kushoto) akitoa maelezo kupitia ramani inayoonesha muonekano wa Kijiji cha Msomera mara baada ya kupangwa.
Baadhi ya Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Wakifuatilia kwa makini mazungumzo wakati wa kikao na Mkuu wa Wilaya ya Handeni.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Albert Msando (mwenye tai nyekundu) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Kushoto kwa Mkuu wa Wilaya ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Prof. Wakuru Magigi.