Habari

Vijiji 120 katika Halmashauri za Wilaya 15 kufanyiwa Tathmini na Ukaguzi

Vijiji 120 katika Halmashauri za Wilaya 15 kufanyiwa Tathmini na Ukaguzi
Nov, 22 2024

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeanza kazi ya kufanya Tathmini na Ufuatailiaji (Monitoring and Evaluation) ya utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa pamoja na Uzingativu (Compliance) wa Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Halmashauri za Wilaya mbalimbali nchini.

Tume imesambaza wataalamu wake katika Halmashauri za Wilaya 15, kwenye Mikoa 15 ili kutekeleza jukumu hilo kwenye Vijiji vilivyowezeshwa na Tume kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kazi hiyo itakayochukua takribani wiki tatu, inavigusa Vijiji 120 katika Halmashauri za Wilaya za Makete (Njombe), Mbarali (Mbeya), Mufindi (Iringa), Tunduru (Ruvuma), Rufiji (Pwani) Buhigwe (Kigoma), Mpwapwa (Dodoma) na Misingwi mkoani Mwanza.

Aidha, Halmashauri nyingine zitakazohusika na zoezi hilo ni pamoja na Bukoba (Kagera), Muheza (Tanga), Shinyanga DC (Shinyanga), Kilosa (Morogoro), Uyui (Tabora), Meatu (Simiyu) na Iramba mkoani Singida.

Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Sura 116, mojawapo la jukumu la Tume ni kufanya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ikiwa ni kuangalia utekelezaji wa mipango hiyo katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali.

Vilevile, Sheria hiyo pia inaitaka Tume kukagua utaratibu uliotumika katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi Kama ulifuata Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayotumika katika hatua za uandaaji wa mipango hiyo.

Kukamilika kwa kazi hizo hutoa mwanga endapo kunahitajika maboresho yeyote yatakayosaidia Mamlaka za Upangaji na Wadau mbalimbali katika zoezi zima la Uandaaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.