Habari
Vijiji 333 katika Halmashauri za Wilaya 21 kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya 21 zilizopo kwenye Mikoa 14 inatarajia kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 333 kupitia Programu ya Upangaji Matumizi ya Ardhi ya Vijiji iliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Uandaaji wa mipango hiyo unalenga katika maeneo yanavyopitiwa na miradi ya Kitaifa ya Kimkakati ikiwemo Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na Reli ya Kisasa (SGR), Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) pamoja Wilaya na Vijiji vyenye vyanzo vya maji vinavyotiririsha kuelekea Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP).
Vilevile, uandaaji wa mipango hiyo ya matumizi ya ardhi inatarajiwa pia kugusa baadhi ya Wilaya na Vijiji vilivyokuwa na migogoro na maeneo ya Hifadhi na ambavyo vilitolewa maamuzi na Baraza la Mawaziri. Aidha, Wilaya na Vijiji vingine vitakavyonufaika na mipango hiyo ni Vijiji vilivyopo mipakani mwa nchi jirani na Tanzania na vile vinavyopitiwa na Mradi wa Bomba la Gesi asilia.
Katika awamu ya kwanza, jumla ya Halmashauri za Wilaya 7 za Manyoni (Singida), Mtwara (Mtwara), Kilindi (Tanga), Mpimbwe (Katavi), Korogwe (Tanga), Ukerewe (Mwanza) na Ushetu Mkoani Shinyanga zitahusika na zoezi hilo lililoanza Aprili 3, 2025.
Aidha, awamu ya pili ya zoezi hilo itahusisha Halmashauri za Wilaya ya Tandahimba (Mtwara), Igunga (Tabora), Bukombe (Geita), Sikonge (Tabora), Mpwapwa (Dodoma), Magu (Mwanza), na Ikungi katika Mkoa wa Singida.
Zoezi hilo litakamilika kwa awamu ya tatu itakayohusisha Vijiji vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya ya Masasi (Mtwara), Kishapu (Shinyanga), Sengerema (Mwanza), Kalambo (Rukwa), Ruangwa (Lindi), Iramba (Singida) pamoja na Lushoto Mkoani Tanga.
Kazi hiyo inayowezeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo inafanyika ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoitaka Wizara kupitia Tume kukamilisha Programu ya uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 333 kabla ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 kumalizika mnano Juni 30, 2025.