Habari
Vijiji Loliondo Kupimwa na kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imeanza kazi ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiji 14 vilivyoko kwenye kata 8 katika Tarafa ya Loliondo. Kazi hii pia itahusisha upimaji wa mipaka ya Vijiji, utoaji wa vyeti vya ardhi ya vijiji, uandaaji wa Mipangokina pamoja na utoaji wa Hatimiliki za Kimila kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha maandalizi ya kazi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mh. Raymond Steven Mwangwala ameishukuru Serikali kwa kusikia ombi la wananchi wa Vijiji hivyo kwani kwa nyakati tofauti wamefika ofisini kwake kuleta maombi ya kupimiwa vijiji vyao. Aidha, Mkuu wa Wilaya amesema uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi utasaidia wananchi wa vijiji hivyo kutumia ardhi kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali ili kuleta mafanikio katika nyanja za kiuchumi na kijamii sambamba na kuhifadhi mazingira.
Mbali na hilo, naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Dkt. Jumaa Mhina amesema kuwa zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji hivyo itasaidia kuwahakikishia wananchi umiliki wa ardhi za vijiji pamoja na kuondoa migogoro ya mipaka baina ya kijiji na kijiji.
“Zoezi la Upimaji na Upangaji wa Vijiji hivi pia litasaidia kuondoa migogoro ya ardhi na dhana potofu kuwa Serikali ina mpango wa kuchukua maeneo yao kwa kuwa Vijiji vinaenda kupata vyeti vya ardhi vitakavyowasaidia kuwa na uhakika wa umiliki wa ardhi yao” alisema Dkt. Jumaa Mhina
Awali, akitoa maelezo ya kazi hiyo, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu, Bw. Jonas Masingija Nestory kutoka Tume amesema kuwa kazi hiyo imegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu hizo ni Upimaji wa mipaka ya Vijiji, Utoaji wa Vyeti vya Ardhi vya Vijiji, uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Uandaaji wa Mipangokina ambao utahusisha kupima vipande vya ardhi na kutoa Hatimiliki za Kimila.
“Sambamba na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, pia kutakuwa na upimaji wa mipaka ya vijiji, lengo ni kuwa kila kijiji kujulikana mipaka yake, kubainisha matumizi mbalimbali yaliyopo kwenye kila kijiji, ikiwa ni pamoja na maeneo ya makazi, kilimo, malisho, hifadhi za misitu na vyanzo vya maji, ili kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili hapo awali” alisisitiza Bw. Masingija.
Kikao hicho kilihusisha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wataalamu kutoka Tume na Halmashauri ya Wilaya, pamoja na Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji. Lengo la kikao hiki ilikuwa ni kujenga uelewa kwa Uongozi wa Wilaya pamoja na Vijiji juu ya zoezi la uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mh. Raymond Stephen Mwangwala (katikati) akizungumza katika kikao cha maandalizi ya uandaaji wa Mipango wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji.
Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu (DLUPMC) kutoka Tume Bw. Jonas Masingija Nestory akitoa maelezo juu ya dhana ya uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lopoluni (aliyesimama) akiwasilisha hoja wakati wa kikao cha maandalizi ya kazi ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuken (aliyesimama) akiuliza swali kwa ajili ya kupata ufafanuzi juu ya kazi ya uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Kijiji chake.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ngorongoro wakifuatilia kwa makini majadiliano juu ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji.
Baadhi ya Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao.
Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji wakifuatilia mjadala wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya vijiji.
Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro mara baada ya kuhitimisha kikao cha Maandalizi ya kuwezesha Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 katika Tarafa ya Loliondo, Wilayani Ngorongoro.