Habari

Vijiji Simiyu Kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wananchi Kupatiwa Hatimiliki

Vijiji Simiyu Kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Wananchi Kupatiwa Hatimiliki
Mar, 27 2023

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya ya Busega, Itilima na Meatu inatarajiwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji 25 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na Mapori ya Akiba ya Maswa na Kijereshi ili kuimarisha uhifadhi na kuwawezesha wananchi wa vijiji hivyo kuwa na milki salama.

Akizungumza na wataalamu katika kikao cha maandalizi ya kazi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume Prof. Wakuru Magigi amewataka wataalamu hao kufanya kazi kwa bidii na kuweka mbele uzalendo, ustawi wa wananchi pamoja na maslahi mapana ya Taifa ili kuondoa migogoro ya ardhi, kulinda uhifadhi na kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi ili kuboresha maisha yao.

“Tunaenda kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji katika Halmashauri tatu, (Meatu, Busega na Itilima) mkiwa kazini kila mtu akawajibike kwenye eneo lake, mkafanye kazi kwa ushirikiano ili kuleta kazi yenye ubora na tija itakayosaidia wananchi na Taifa kwa ujumla” alisema Prof. Magigi.

Aidha, Prof. Magigi aliwaasa Wataalamu hao kuzingatia maelekezo ya Viongozi kwani baadhi ya vijiji vitakavyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ni miongoni mwa vijiji 975 vilivyokuwa na migogoro na hifadhi, na ambavyo maamuzi yake yalikwishatolewa na Baraza la Mawaziri.

“Kati ya vijiji hivi 25 tunavyoenda kuvifanyia kazi, kuna baadhi ya vijiji vimeshatolewa maamuzi na Baraza la Mawaziri, hivyo kila kijiji mnachoenda, lazma muangalie viongozi walitoa maelekezo gani juu ya vijiji hivyo, na maelekezo hayo ya viongozi inabidi yazingatiwe kwenye mpango wa matumizi ya ardhi wa kila kijiji husika” alisisitiza Prof. Magigi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu (DLUPMC) Bw. Jonas Masingija Nestory aliwataka wataalamu hao kuwaongoza wananchi kutenga matumizi ya ardhi ambayo ni rafiki na uhifadhi kwani itasaidia jamii kufanya shughuli zao bila kuwa na migogoro na hifadhi.

Aidha, Mkurugenzi Masingija aliwaeleza wataalamu hao kuwa, mara tu baada ya kukamilika kwa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi itafuata hatua ya kuandaa Mipango Kina (Detail land use plans) ambapo wananchi watapimiwa maeneo yao na kupatiwa Hatimiliki za Kimila ili kuwa na uhakika wa kumiliki ardhi.

“Wakati wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi mkazingatie utengaji wa matumizi ya ardhi ambayo ni rafiki na uhifadhi, kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa migogoro iliyokuwa ikijitokeza mara kwa mara kati ya hifadhi na vijiji au wanyamapori na wananchi (human-wildlife conflict) alisema Bw. Masingija.

Utekelezaji wa kazi hiyo unategemewa kushirikisha Wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Hifadhi la Taifa, (TANAPA), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na Shirika la Uhifadhi la FZS. Aidha, kazi hiyo ni muendelezo wa malengo ya Serikali katika kuimarisha uhifadhi, kuondoa migogoro ya ardhi kwenye Vijiji vinavyopakana na Hifadhi na kuwezesha milki salama kwa wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume Prof. Wakuru Magigi akiongea na watumishi (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa kazi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 25 mkoani Simiyu


Sehemu ya Watumishi wa Tume waliohudhuria kikao wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Tume

Wataalamu kutoa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) na Shirika la Uhifadhi la FZS wakiwa kwenye kikao cha pamoja kukamilisha maandalizi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji mkoani Simiyu.

Msafara wa Wataalamu wa Tume ukiwa njiani kuelekea Halmashauri za Wilaya ya Itilima, Meatu na Busega Mkoani Simiyu kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji katika Halmashauri hizo