Habari
Viongozi, Wananchi Nyang'hwale Waipongeza Tume uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuzunguka Msitu wa Hifadhi
Eneo lenye Hekta 1,296 ya zilizokuwa za Hifadhi ya Msitu wa Mienze katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita zimetengwa na kupangiwa matumizi mbalimbali kwa ajili ya wananchi huku, Hekta nyingine 7,692 zikipimwa na kuachwa kwa ajili ya Uhifadhi endelevu ikiwa ni utekelezaji wa Maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusu Msitu huo wa Hifadhi.
Hayo yamebainika wakati Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) pamoja na wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale wakihitimisha zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 vikiwemo Vijiji vya Bujala Mienze, Shabaka, Wavu na Ihushi vinavyopakana na Msitu wa Hifadhi wa Mienze uliopo ndani ya Halmashauri hiyo.
Wakizungumza mara baada ya kupitisha mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji vyao kwenye mikutano ya Vijiji, baadhi ya wananchi wa Vijiji hivyo wameishukuru Serikali kwa kuwaletea zoezi hilo ambalo wamesema litakuwa ni suluhisho la migogoro ya matumizi ya ardhi pamoja na kuwawezesha kulinda uhifadhi na kujiletea maendeleo.
“Kwa kweli tunashukuru, Kijiji chetu kimepata ekari 331, wananchi wameweza kupata maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile maeneo ya makazi, kilimo, pamoja na malisho. Eneo hili lililoongezeka litatusaidia pia kupunguza makazi ya msongamano, kwani watu watapita maeneo mapya ya ujenzi, na pia itachangia watu wasivamie kwenye hifadhi” alisema Bw. Masikitiko Paulo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihushi.
Awali, akizungumza katika Mkutano wa Kijiji cha Ihushi, Mpima Ardhi Mwandamizi kutoka Tume Bw. Hemed Mzule amewaasa wananchi hao kutumia vizuri maeneo hayo yaliyomegwa kutoka kwenye Hifadhi kwani mara baada ya kuyatoa maeneo hayo, Msitu huo tayari umepimwa na kuhifadhiwa na hakuna shughuli ya kibinadamu itakayoruhusiwa ndani ya Msitu huo.
Aidha, kwa upande wa wananchi wa Kijiji cha Nyashilanga, wamesema kuwa mpango wa matumizi ya ardhi ulioandaliwa Kijijini kwao umekuja wakati muafaka kwa kuwa utawasaidia kuondoa muingiliano baina ya makundi mbalimbali ya watumiaji ardhi ambao umedumu Kijijini hapo kwa muda mrefu.
“Zoezi hili limekuja kwa wakati sahihi, kwa kipindi cha nyuma tumekuwa na migogoro mingi sana ila kwa ujio wa zoezi hili la upangaji wa ardhi nafikiri itakuwa tiba kwa matatizo yaliyopo kwenye kijiji chetu, maana ukiangalia, wafugaji waliokuwa wanaingiza mifugo kwenye maeneo ya kilimo, ila kwa mpango huu na hizi Sheria tulizojiwekea, hilo linaenda kuisha,” alisisitiza Bw. Faustine James, Mkazi wa Kijiji cha Nyashilanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Bw. Vitalis Ndunguru ambaye pia ni Katibu Tawala Wilaya hiyo, ameeleza kuwa zoezi lililofanyika litakuwa na faida kubwa kwa wananchi kwani hapo awali kulikuwa na uvamizi mkubwa Msituni ila kwa sasa watakuwa na ufahamu wapi wanafanya shughuli zao na wanaishia wapi hali itakayoondoa migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Ndg. Husna Toni ameipongeza Serikali kupitia Tume kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji hivyo kwani zoezi hilo limegusa mpango mkakati wa Halmashauri hiyo ya kuongeza kipato kupitia Msitu wa Hifadhi pamoja na kukuza kilimo cha umwagiliaji.
“Wilaya inategemea kuwa na miradi mikubwa miwili, kwanza ni utunzaji wa mazingira kupitia uhifadhi wa Msitu wa Mienze, ambapo tunategemea kutumia msitu kufanya biashara ya hewa ukaa lakini pia kuulinda msitu huo ili kusifanyike shughuli za kibinadamu” alisisitiza Ndg. Toni na kuongeza “lakini pia tunalo Bwawa la Nyamgogo ambalo sisi kama Halmashauri tunategemea kutengeneza mradi mkubwa wa umwagiliaji, sasa ili tufanikiwe kwa yote haya ni lazma tuandae mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji vinavyozunguka hii miradi”
Mkurugenzi huyo pia ameeleza nia ya Halmashauri hiyo kuendelea kushirikiana na Tume ili kuhakikisha Vijiji vyote 62 vya Wilaya hiyo vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara kutokana na uwepo wa shughuli mtambuka zikiwemo za uchimbaji madini.
Naye Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bw. Mathias Bujiku ameeleza mafanikio makubwa ya zoezi hilo kutokana na muitikio na ushirikiano walioupata kutoka kwa wananchi wa Vijiji hivyo. Aidha, Bw. Bujiku, amewataka wananchi hao kuheshimu mipango hiyo wakati wa utekelezaji huku wakisubiri muendelezo wa zoezi hilo utakaowapelekea kupata Hati za Hakimiliki za Kimila na kumiliki maeneo yao Kisheria.
Msitu wa Hifadhi wa Mienze ulianzishwa ukiwa na ukubwa wa eneo la Hekta 8,988, mara baada ya uvamizi na kuanza kufanyika kwa shughuli za kibinadamu kwenye sehemu ya Msitu huo, ndipo Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ya Baraza la Mawaziri ilifanya maamuzi ya kuwaachia wananchi sehemu ya eneo la Msitu huo lenye ukubwa wa Hekta 1,296, na kuhifadhi eneo lililobakia la Hekta 7,692 kwa ajili ya Uhifadhi endelevu ili kunusuru Msitu huo kutokutoweka.
Kufanyika kwa kazi hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume kupitia fedha za miradi ya maendeleo. Mradi huo umejikita katika Vijiji vilivyopo kwenye Wilaya zinazopitiwa na Miradi ya Kimkakati, Wilaya zilizopo mipakani na nchi jirani, pamoja na Vijiji vyenye Migogoro ya matumizi ya Ardhi.