Habari

Wananchi Mtakuja wanufaika na Hatimiliki kupitia Mradi wa Uhifadhi Misitu ya Miombo

Wananchi Mtakuja wanufaika na Hatimiliki kupitia Mradi wa Uhifadhi Misitu ya Miombo
Jan, 14 2025

Na Claudius Masayanyika, Mlele, Katavi

Wananchi zaidi ya 200 wa Kijiji cha Mtakuja wananchi wa Kijiji cha Mtakuja kilichopo Kata ya Nsenkwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mkoani Katavi wamenufaika na Hati za Hakimiliki za Kimila (CCRO’s) mara baada ya Kijiji chao kuandaliwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi uliopelekea kupimiwa maeneo yao na kuandaliwa Hati hizo.

Akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa Hatimiliki hizo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga amesema, Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyoandaliwa katika Vijiji 6 vya Wilaya hiyo imewezesha kuwajengea uwezo wadau katika kusimamia rasilimali za misitu na kutatua migogoro baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa.

Aidha Majid, amesema mradi huo umewezesha utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Baraza la Mawaziri juu ya Migogoro ya Ardhi, kwa kuwa Kijiji cha Mtakuja kilikuwa ni miongoni mwa Vijiji 975 vilivyokuwa na migogoro ya ardhi kati ya Hifadhi na Wananchi.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema, kufikia hatua ya kupima na kutoa Hatimiliki kufanya itasaidia Wananchi kuwa na Milki salama za Ardhi zao pamoja na kuondokana na migogoro ambayo imekuwa ikiibuka kila mara. Aidha, amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwa na Mlele iliyopangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa kila kipande cha ardhi kinachomilikiwa na wananchi ama Taasisi.

Mkuu wa Wilaya ya Mlele ameishukuru Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuendesha zoezi hilo ambalo lina manufaa makubwa kwenye Wilaya yake.

Zoezi hilo limefanyika chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Kimataifa (GEF) na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Miombo - DSL IP unaotekelezwa na TFS.