Habari

Waziri Mkuu atoa wito kwa Taasisi za Kifedha kuzitambua Hati za Kimila

Waziri Mkuu atoa wito kwa Taasisi za Kifedha kuzitambua Hati za Kimila
May, 30 2024

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuzitambua hati za kimila kama dhamana ya kutoa mikopo kwa wananchi.

Amesema kuwa hati zote zinazotolewa na Wizara au za kimila zinatambulika kisheria na zina fursa kwa mwenye hati hiyo kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za kifedha.

Ametoa wito huo Bungeni leo (Alhamisi, Mei 30, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itabadili Sheria ya Ardhi ili watu wa vijijini watumie hati za kimila kupata mikopo.

Ameongeza kuwa inawezekana zipo taasisi za kifedha ambazo hazikubali hati hizo kwasababu ya matakwa au mpango kazi wao, lakini kwa mujibu wa Sheria hati hizo ni halali na zinatolewa kisheria kwa vipindi kama ilivyo zile zinazotolewa na Wizara kwa miaka 33, 66 hata 99

“Nitoe wito kwa Taasisi zote za kifedha ambazo zimeridhiwa na Serikali kufanya shughuli zake nchini kwa mujibu wa Sheria za nchi ziendelee kutumia na kutoa fursa kwa wenye hati za kimila au zinazotolewa na Wizara ya Ardhi kuwa ni hati halali zinatambulika na zinatoa fursa kwa mtanzania anayemiliki ardhi nchini kupata mkopo”

Hati za Hakimiliki za Kimila hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji na huandaliwa kwenye ardhi ya Vijiji mara baada ya Vijiji husika kukamilisha zoezi la Upangaji Matumizi ya Ardhi kwenye Vijiji husika.