Habari

Waziri wa Ardhi azindua Bodi ya Tume

Waziri wa Ardhi azindua Bodi ya Tume
Apr, 24 2018

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amezindua rasmi Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi leo tarehe 15 Oktoba 2016. Kamisheni ya Tume ambayo Waziri ameizindua leo ina Makamishna sita ambao wameteuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoka sekta za umma, sekta binafsi na sekta za kijamii. Tukio hili limefanyika mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kumteua Fidelis Mutakyamilwa kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni kuanzia Agosti 26, 2016.

Makamishna wanaounda Kamisheni hiyo Bw. Paulo M. Tarimo (Mkurugenzi Idara ya Mipango ya Mjatumizi ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi), Bw. Denis I. Bandisa (Mkurugenzi –TAMISEMI), Bi. Sarah A. Kyessi (Sekta Binafsi), Dkt. Nebbo J. Mwina (Mkurugenzi Kitengo cha Wanyamapori – Wizara ya Maliasili na Utalii), Eng. Seth Phili Lusema (Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiiliaji) na Bi. Florence Maridadi Mwanri (Katibu Mtendaji Msaidizi Tume ya Mipango). Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka 2007, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume Dkt Stephen J. Nindi ndiye anakuwa Katibu wa Kamisheni.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Waziri ameiagiza Kamisheni hii mpya kusimamia shughuli za Tume na kuhakikisha kwamba Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi inakidhi matarajio ya wananchi na kuleta tija na mahusiano mazuri kwa wadau wote wa mipango ya matumizi ya ardhi.