Habari
Wenyeji Msomera waanza kunufaika na umilikishwaji ardhi
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, imeanza zoezi la umilikishaji ardhi katika maeneo ya Makazi na Kilimo kwa wenyeji waishio katika Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Tume anayeshughulikia Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Obed Katonge amesema kuwa wataalamu kutoka Tume wameweka kambi katika kijiji hicho ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kama ilivyokusudiwa na Serikali.
“Tumepiga kambi hapa kijijini Msomera kutimiza azma ya Serikali kuhakikisha wananchi wote wakiwemo wenyeji na wageni wanapimiwa ardhi na kumilikishwa na hilo tutahakikisha linatimia kwa usahihi na viwango.” alisema Bw. Katonge.
Aidha, Bw. Katonge alitambua ushirikiano mkubwa walioupata kuanzia ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri ya Wilaya pamoja na wenyeji wa kijiji cha Msomera. Alielezea hatua hiyo kama chachu ya kufanikiwa kwa zoezi hasa ukizingatia utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni jambo linalohitaji ushirikishwaji wa ngazi zote katika Mamlaka za upangaji.
“Tumepata mapokeo mazuri kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wananchi pia wanaishukuru Serikali na kutoa ushirikiano kwa wataalam jambo ambalo linatupa taswira ya ukamilifu wa zoezi hili utakuwa mzuri” alisema Katonge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkababu kilichopo katika kijiji cha Msomera Yohanna Mapashi amesema zoezi hilo linakwenda kutatua changamoto za migogoro ya Ardhi baina ya wenyeji na wageni waliohamia kijijini hapo kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwani wenyeji walikuwa na hofu ya kupoteza maeneo yao jambo ambalo lilipunguza ushirikiano baina yao.
“Tulikuwa tunadhani tumesahaulika na Serikali, watu walikuwa na hofu ya kuchukuliwa maeneo yao sababu tulikuwa ni kama tumevamia japo tumeishi kwa muda mrefu huku (Msomera), sasa tunapoona Serikali imetukumbuka na sisi tunapimiwa na kugawiwa maeneo kwakweli tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita na tunamshukuru sana Mh. Rais kwa kutuletea wataalam” alisema Mapashi.
Hapo awali, Kijiji cha Msomera kilianzishwa ndani ya lililokuwa Pori Tengefu la Handeni lililovamiwa na wananchi na kuanzisha kijiji hicho. Hata hivyo, Serikali iliamua kufuta Pori hilo, ambapo kwa sasa linakaliwa na wenyeji wa kijiji hicho na wageni waliohamia kwa hiari yao kutoka kwenye Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (katikati) wakihakiki taarifa za kijiografia katika maeneo yanayopimwa kwa ajili ya kumilikishwa wananchi wa kijiji cha Msomera
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Msomera Peter Swakei akijaza fomu ya maombi kwa ajili ya kumilikishwa ardhi.
Mkurugenzi Msaidizi – Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Obed Katonge (wa pili kulia) akihakiki fomu za maombi za umilikishwaji wa ardhi kwa wananchi wa kijiji cha Msomera.